Mamia
 ya wafanyakazi katika mashirika na taasisi mbalimbali za umma 
zinazoendeshwa kwa hasara likiwamo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) 
wako hatarini kufutwa kazi kufuatia amri ya serikali  ya awamu ya
tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji katika taasisi hizo.
tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji katika taasisi hizo.
Mashirika
 hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi wengi, lakini bado 
uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.
Hayo
 yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili wa  Hazina,  Laurence 
Mafuru,  katika kikao na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa taasisi na 
mashirika ya umma.
“Kuna
 kampuni ambazo zimepewa mtaji na serikali, lakini zinashindwa 
kuzalisha. Zinaandika barua kuomba msaada Serikali Kuu. Kama unaona 
(mkuu wa taasisi) una wafanyakazi wengi na huzalishi kwa namna 
inayotarajiwa, ni vyema upunguze watu,” alisema Mafuru.
Kadhalika,
 licha ya kutoa maelekezo hayo, Mafuru alizitaja taasisi kadhaa 
zinazoendeshwa kwa hasara au kuzalisha chini ya kiwango kinachotarajiwa 
kuwa ni Tanesco, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Kampuni
 ya Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege (ATCL), Kampuni ya Simu 
Tanzania ( TTCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Maafuru
 alizitaja taasisi na mashirika mengine yasiyofanya vizuri kuwa ni 
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Bandari (TPA), 
Kampuni ya Miliki ya Rasilimai za Reli (Rahco) na Chuo cha Usimamizi wa 
Fedha (IFM).
Mafuru
 alisema Serikali haihitaji kuvuna fedha katika taasisi hizo, bali jambo
 kubwa ni kuona kuwa zinajiendesha na kutimiza malengo yanayotarajiwa na
 umma wa Watanzania.
“Serikali
 haihitaji kuchukua fedha katika taasisi hizi. Isipokuwa tunataka 
(taasisi za umma) zifanye kazi na ziwe nguzo za uchumi wa nchi. Tuache 
bajeti inayotengwa (na serikali) ifanye kazi nyingine ya maendeleo kwa 
Watanzania,” alisema, huku akiyataja Tazara na TRL kuwa ni vinara wa kuomba fedha kwa Serikali Kuu ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.
“Kwa
 mfano Tanesco, kwa kipindi chote ilichoanza kufanya kazi mpaka sasa 
tulitarajia iwe imefanya kazi nzuri ya uzalishaji, lakini badala yake 
tunaona kinyume chake na hapo isitegemee kwamba endapo itaendelea 
kufanya hivyo serikali itakuwa inaangalia tu,” alisema.
“Ni
 vema kama kuna shirika au taasisi ya umma ambayo inaona haizalishi na 
ina wafanyakazi wengi iwapunguze wafanyakazi hao. Kama tunaona 
tunashindwa, ni vyema tupunguze watu au turudi nyumbani tukapumzike,” alifafanua Mafuru.
Mafuru
 aliongeza kuwa baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa taasisi na 
mashirika ya umma ni uzembe wa baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi 
kwa kiwango kinachotarajiwa na wala kuwajibika ipasavyo katika kutimiza 
majukumu yao.
Alisema
 tatizo jingine ni viongozi wa baadhi ya taasisi na mashirika hayo ya 
umma kuchukulia nafasi za uteuzi wanazopewa kuwa ni zawadi, fikra ambazo
 hivi sasa wanapaswa kuzifuta mara moja na kutanguliza zaidi uwajibikaji
 hasa kwa kutambua kuwa serikali ya awamu ya tano inaangalia zaidi 
utendaji wenye matokeo chanya kwa umma na siyo kinyume chake.
“Msifikiri
 kwamba nyie ndiyo wapishi (wajuzi) pekee… wapo watu wengine wanaojua 
zaidi, kwa hiyo mjiandae kufanya kazi. Kila mtu atawajibika kwa nafasi 
yake,” alisema.
Alisema 
 pamoja na kwamba serikali imezipa mali  taasisi hizo kujiendesha, 
lakini zimendelea kuwa mzigo kwa serikali kwani baadhi hushindwa 
kuzalisha na kuwa vinara wa ‘kutembeza bakuli’ kwa maana ya kuomba 
msaada kwa Serikali Kuu mara kwa mara.
Mafuru
 alikitaja Chuo cha IFM kuwa ni mojawapo ya taasisi za serikali 
zinazoshangaza kwani licha ya kuwa na fursa ya kuzalisha, bado kimekuwa 
kikiendeshwa kwa hasara na kuwa miongoni mwa vinara wa kuomba msaada kwa
 Serikali Kuu.
“Kwa
 mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana na ada za 
wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?”alihoji.
Alisema
 taasisi zinazojiendesha kwa hasara zimekuwa mzigo mzito kwa serikali, 
hivyo ni lazima sasa kwa wakuu wa taasisi husika kuhakikisha kuwa 
wanaongeza ufanisi ili kujikwamua kutoka katika hali mbaya kiuchumi 
waliyonayo.
“Hivi
 sasa serikali ina taasisi 220 kutoka 600 zilizokuwapo awali. Pamoja na 
kwamba taasisi za serikali zimepewa assets (mali) za kuzalisha, bado 
(baadhi) zimeshindwa kufanya hivyo, badala yake nyingine kila siku 
zinaandika barua kuomba fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali kuongezewa 
mtaji,” alisema.
Katika
 hatua nyingine, Mafuru alisema inasikitisha kuona kuwa Mamlaka ya 
Bandari Tanzania (TPA) ni miongoni mwa taasisi zisizozalisha kwa kiwango
 kinachotarajiwa na kwamba hadi sasa, hakuna faida yoyote ambayo imekuwa
 ikirudisha serikalini.
Alisema kama TPA inafanya vizuri, ilitakiwa kufanya maendeleo mengine ikiwamo kujenga bandari nyingine.
Aliitaka taasisi hiyo na nyinginezo kama TPDC kujifunza kutoka kwa taasisi binafsi juu ya namna ya kuongeza uzalishaji.
Alisema
 kutokana na uendeshaji wa hasara kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya 
umma, matokeo yake mashirika na taasisi hizo, kwa pamoja huchangia 
asilimia 22 tu ya pato la Taifa kwa mwaka, hali ambayo haipaswi 
kuendelea.
Wakati
 huo huo, Mafuru alitoa agizo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za 
Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa taasisi za umma ifikapo 
Desemba 15, zikiwamo zote zilizobainika kuwa hazikuwa zikifanyiwa 
ukaguzi hapo kabla.
 






 
 
0 comments:
Post a Comment